Tarehe 21 Juni, 2026 Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Agnes Kayola, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Crispin Francis Chalamila jijini Lilongwe, Malawi.
Mhe. Balozi Kayola alimfahamisha Mkurugenzi Mkuu kuwa Ubalozi unatambua jitihada zinazofanywa na TAKUKURU katika kuongoza mapambano dhidi ya rushwa nchini hususan katika kuzuia rushwa, hatua ambayo inalenga kudhibiti ubadhirifu na kuboresha huduma za jamii.
Aidha, Mhe. Balozi alieleza kuwa Ubalozi unaendelea vyema na majukumu yake ikiwemo utekelezaji wa diplomasia ya uchumi. Baadhi ya majukumu aliyoyabainisha ni pamoja na kufanikisha utiaji saini wa Mkataba wa Mfumo wa Urahisishaji wa Ufanyaji Biashara (Simplified Trade Regime- STR) kati ya Tanzania na Malawi; maandalizi ya uratibu wa Kongamano la Tatu la Biashara kati ya Tanzania na Malawi linalotarajiwa kufanyika tarehe 29 hadi 31 Julai, 2026 jijini Dar es Salaam; na uratibu wa Kambi ya matibabu ya kibingwa na bobezi itakayofanyika mwanzoni mwa mwezi Julai, 2026 nchini Malawi ikihusisha Madaktari kutoka hospitali ya Benjamin Mkapa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU, alimpongeza Mhe. Balozi kwa jitihada zake za kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa kutafuta fursa za biashara na uwekezaji kwa manufaa ya Taifa.