Mkutano wa Nne wa Kamati ya Siasa na Diplomasia ya SADC (ISPDC) ngazi ya Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje umeanza rasmi tarehe 28 Aprili 2026 mjini Salima, Malawi, Mkutano huo wa siku mbili unajadili ajenda mbalimbali ikiwemo kufanya tathmini ya utekelezaji wa maamuzi ya Mikutano ya Wakuu wa Nchi na serikali, hali ya Ulinzi na Usalama katika kanda; hali ya uimarishaji wa demokrasia katika kanda; na masuala ya usuluhishi na utatuzi wa migogoro katika kanda.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo unaongozwa na Mheshimiwa Balozi Agnes R. Kayola, Balozi wa Tanzania nchini Malawi akimwakilisha Balozo Dkt. Samwel W. Shelukindo, Katibu Mkuu, Wizara Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Akizungumza katika Mkutano huo, Balozi Kayola ametoa wito kwa Nchi Wanachama na Jumuiya kuendelea kutumia njia za kidiplomasia, katika udhibiti na utatuzi wa migogoro inayojitokeza katika kanda.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa Nchi Wanachama ketekeleza maamuzi yanayofikiwa na viongozi kama nyenzo muhimu ya kuimarisha umoja na mshikamano katika kanda. Sambamba na hilo, alipongeza juhudi za uhifadhi wa historia ya Harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika zinazofanywa na kanda kupitia Mradi wa Hashimu Mbita.