Tarehe 20 Mei 2026, Mhe.Agnes Richard Kayola, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Malawi alitembelea Chuo Kikuu cha Malawi (UNIMA) na kufanya mazungumzo na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Samson Sajidu pamoja na baadhi ya wahadhiri waandamizi katika idara ya lugha. Lengo la mazungumzo hayo lilikuwa ni kuweka mikakati ya namna ya kushirikiana katika kuandaa maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani yanayofanyika tarehe 7 Julai kila mwaka. Mhe. Balozi Kayola alishukuru uongozi wa UNIMA kwa kuanzisha somo la lugha ya Kiswahili ambapo ilielezwa kwa sasa chuo kina jumla ya wanafunzi 17 wanaosoma lugha hiyo kwenye Idara ya Lugha. Aidha, Mhe. Balozi Kayola alishukuru uongozi wa UNIMA kwa kuendelea kushirikiana katika kuiendeleza na kuikuza lugha ya Kiswahili nchini Malawi ambapo ni utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024 inayosisitiza utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ikiwemo kutumia lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya Diplomasia ya Uchumi. Aidha, kwa upande wake Prof. Sajidu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Malawi alimpongeza Mhe. Balozi Kayola kwa jitihada zake za kuikuza na kuindeleza lugha ya Kiswahili nchini Malawi, hatua ambayo ameeleza itaongeza watumiaji wa lugha hiyo na hivyo kuimarisha zaidi mashirikiano kati ya Tanzania na Malawi. Vilevile, Prof Sajidu alieleza kuwa pamoja na mafanikio waliyopata katika kuanzisha programu ya Kiswahili chuoni hapo, zipo baadhi ya changamoto ikiwemo kukosekana kwa maabara ya lugha chuoni hapo pamoja na upatikanaji wa madarasa kwa njia mtandao. Pamoja na hayo, UNIMA imepongeza ushirikiano uliopo kati yake na Ubalozi wa Tanzania. Vilevile Mhe. Balozi ameahidi kuwaleta nchini Tanzania wanafunzi watakaofanya vizuri katika mitihani ya somo la Kiswahili kutembelea Chuo Kikuu Mzumbe ambacho UNIMA wana mkataba wa miaka minne (4) wa kubadilishana utaalam katika ufundishaji wa lugha ya Kiswahili.