Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya kutoka Tanzania Dkt. Ntuli Kapologwe, aliibuka mshindi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati, na Kusini (ECSA – HC) na kuwashinda wagombea wengine sita waliokuwa wakiwania nafasi hiyo. Dkt. Ntuli alipitishwa kushika nafasi hiyo katika Mkutano wa Mawaziri wa Afya wa 74 wa Nchi Wanachama wa ECSA-HC, uliofanyika kuanzia tarehe 10 hadi 12 Februari, 2025 Lilongwe, Malawi.
Dkt. Ntuli anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Prof. Yoswa Dambisya, Raia wa Uganda ambaye amehudumu kwenye nafasi hiyo kwa mihula miwili mfululizo kwa kipindi cha miaka 10.
Dkt. Ntuli Kapologwe kwa kuzingatia vigezo maalum vilivyowekwa katika makubaliano ya Jumuiya hiyo, ataongoza kwa muda wa miaka mitano.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha zoezi la uchaguzi Februari 12, 2025, Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo na Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama (Mb) alisema kuwa nafasi hiyo ilipotangazwa kwa mara ya kwanza jumla ya waombaji 47 waliwasilisha wasifu wao na kati yao, saba (7) walichaguliwa kuendelea baada ya mchujo wa awali.
Waziri Mhagama alisema mara baada ya usaili uliofanywa na Kamati ya Mkutano wa Makatibu Wakuu wa nchi wanachama, Dkt. Kapologwe alipata alama za juu zaidi na kuingia katika hatua ya mwisho pamoja na wagombea wengine wawili kutoka Kenya na Malawi.
Ameeleza kuwa majina ya wagombea hao watatu yaliwasilishwa kwenye Mkutano wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati, na Kusini (ECSA – HC), ambapo Dkt. Kapologwe ameibuka mshindi.
Kwa ushindi huu ni dhahiri ya kwamba Tanzania inaendelea kuuthibitishia ulimwengu kuwa ina Watalaam wenye sifa stahiki za kushika hatamu za Uongozi kwenye Jumuiya au Mashirika ya Kimataifa na kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya wengi katika uboreshaji wa huduma za Afya.
“Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kushika nafasi hii katika kipindi cha miaka 51 cha Jumuiya hiyo, kwani kwa mara ya kwanza, Mtanzania Dkt. Winny Mpanju alihudumu kama Mkurugenzi Mkuu kati ya mwaka 1983 na 2000. Ni mafanikio makubwa kuona Tanzania inapata nafasi hii tena baada ya miaka 27,” alisema Mhe. Waziri Mhagama.