Tarehe 20 Disemba, 2023, Mheshimiwa Balozi Agnes Richard Kayola, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Malawi amefanya mazungumzo na Bw. Ally Kakomile, Msaidizi wa Katibu Mtendaji wa Ukanda wa Kati (Central Corridor Transit Transport Facilitation Agency – CCTTFA, kwenye Ofisi za Ubalozi, jijini LilongweKatika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Balozi alifahamishwa kuhusu Jamhuri ya Malawi kujiunga na Ukanda huo tarehe 1 Disemba, 2023, na kwamba sasa Jamhuri ya Malawi ipo katika hatua ya kuridhia Mkataba wa kujiunga na Ukanda huu. Hii ni hatua muhimu ikizingatiwa kuwa nchi zetu mbili zina ushirikiano mzuri wa biashara. Bidhaa nyingi zinazoagizwa Malawi zinapitia Bandari ya Dar es Salaam, na kutumia usafiri wa barabara hadi kufika nchini Malawi. 

Sambamba na hilo, Mheshimiwa Balozi alielezwa shughuli za Ukanda wa Kati, mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa na changamoto ambazo zinaendelea kupatiwa ufumbuzi. Baadhi ya mafanikio ni kuanzishwa kwa One Stop Inspection Stations (OSIS) – ambazo zimepunguza gharama na muda wa kusafirisha mizigo kwa njia ya barabara. Kwa sasa magari yanasimamishwa kwenye vituo vitatu tu ikilinganisha na hapo awali ambapo yalikuwa yanasimamishwa katika vituo zaidi ya 55. Aidha, katika vituo hivi, kuna wakala wa huduma zote muhimu kama vile Wizara ya Mambo ya Ndani, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Misitu (TFS), kwa ajili ya kurahisisha taratibu za kusafirisha mizigo.

Kwa upande wa Ubalozi, Mhe. Balozi alimuhakikishia Msaidizi wa Katibu Mtendaji wa Ukanda wa Kati kuwa, utaendelea kufuatilia kwa karibu hatua za uridhiwaji wa mkataba huo kwa upande wa Serikali ya Malawi. Aidha, alimshukuru kwa kuutembelea Ubalozi kwa lengo la kuufahamisha shuguli zinazofanywa na Ofisi yao.

Ukanda wa Kati ni wakala wa kimataifa iliyoundwa mwaka 2006 na nchi wanachama 5 ambao ni: Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Rwanda, Jamhuri ya Uganda na Jamhuri ya Burundi. Makao Makuu ya Sekretarieti ya Ukanda wa Kati yapo Dar es Salaam, Tanzania.

Ukanda wa Kati ulianzishwa kwa lengo la kuratibu juhudi za nchi wanachama za kuhakikisha uratibu na ushirikiano katika usimamizi wa usafiri na usafirishaji unaoziunganisha nchi wananchama wa ukanda huo kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Jamhuri ya Malawi kujiunga kwenye Ukanda huuu itarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu zinazohusu biashara (Makasha mangapi ya mizigo yamepitia bandari yetu, bidhaa zipi zimeingia na kutoka Tanzania na Malawi, magari mangapi ya mizigo yameingia na kutoka Tanzania na Malawi, pamoja na taarifa nyingine muhimu za kibiashara zitakazosaidia kulinganisha urari wa biashara kwa nchi zetu mbili.