Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), aliwasili nchini Malawi, tarehe 25 Februari, 2025 kwa ziara ya kikazi na kushiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi, Ngazi ya Mawaziri, uliofanyika tarehe 26 Februari 2025 Jijini Lilongwe. Mkutano huo, ulitanguliwa na vikao vya wataalam kuanzia tarehe 24 hadi 25 Februari, 2025. Mkutano huo wa ngazi ya mawaziri umefanyika ukiwa ni jukwaa muhimu la kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kiuchumi kati ya Tanzania na Malawi.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kamuzu Banda jijini Lilongwe Mhe. Waziri Kombo alipokewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Malawi, Mhe. Patricia Nangozo Kainga (Mb), na Balozi wa Tanzania Malawi, Mhe. Agnes Richard Kayola.
Mkutano wa Sita wa JPCC umejadili masuala muhimu ya kuendelea kuimarisha Ushirikiano kupitia sekta za biashara, uwekezaji, miundombinu, elimu, afya, ulinzi na usalama, pamoja na fursa zinazopatikana kwenye maeneo ya ushirikiano katika sekta za kipaumbele.
Mkutano huo pia, umefanya tathmini ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano uliopita pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kutatua changamoto mbalimbali. Katika Mkutano huo, Tanzania na Malawi zimeshaini Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Afya na Mkataba wa Kuhamisha Wafungwa, ikiwa ni hatua muhimu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Mhe. Waziri Kombo akiwa ziarani nchini Malawi alipata fursa ya kutembelea Ofisi za Ubalozi iliyopo Jijini Lilongwe kwa lengo la kuzungumza na Watumishi wa Ubalozi, ambapo Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Agnes Richard Kayola alimpatia taarifa kuhusu hali ya mahusiano ya kidiplomasia, uchumi, siasa na usalama kati ya Tanzania na Malawi. Taarifa hiyo ilihusisha pia masuala ya mali za Serikali ya Tanzania zilizopo nchini Malawi, ustawi wa Watumishi wa Ubalozi pamoja na mchango wa Watanzania washio nchini Malawi katika maendeleo ya taifa. Aidha, Mhe. Waziri Kombo alipokea maelezo kuhusu fursa mbalimbali zinazoweza kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili, hususan katika uwekezaji, usafirishaji, biashara za mipakani na utalii.
Akizungumza na Maafisa wa Ubalozi, Mhe. Waziri Kombo alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuitangaza vyema Tanzania katika eneo la uwakilishi na kutumia fursa zilizopo ipasavyo kwa manufaa ya maendeleo ya taifa. Kwa upande wake, Mhe. Balozi Kayola alimshukuru Mhe. Waziri Kombo kwa ziara yake na kuahidi kuwa Ubalozi utaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa masilahi ya nchi yetu.
Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri Kombo aliambatana Mhe. Hamza Hassan Juma, Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu na Baraza la Wawailishi; Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt.Habiba Hassan Omar; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ali Sakila Bujiku.