Tarehe 7 Julai 2023, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya Mazungumzo Rasmi na Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera, Rais wa Jamhuri ya Malawi katika Ikulu ya Kamuzu, Lilongwe. Wakuu wa Nchi hizi mbili walijadili masuala yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa muda mrefu uliopo baina ya Tanzania na Malawi, maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, kutathmini ushirikiano hususan kwenye biashara na uwekezaji, usafiri na usalama wa mipaka na maeneo mengine yenye maslahi mapana kwa nchi zetu mbili.
Waheshimiwa Marais walishuhudia utiaji Saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano Katika Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (Memorandum of Understanding between the Government of the United Republic of Tanzania and the Republic of Malawi in the Area of Telecommunication /Information and Communications Technology. Hati ya Makubaliano ilisainiwa na Mheshimiwa Nape M. Nnauye (Mb), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Moses Kunkuyu (MP), Waziri wa Habari wa Jamhuri ya Malawi.
Baada ya Mazungumzo Rasmi, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Lazarus McCarthy Chakwera walielekea Jiji la Blantyre kutembelea Eneo la Kapeni View Point kuona athari za Kimbunga Freddy kilichotokea mwezi Machi, 2023.